Wakati harakati za kampeni zikiendelea nchini Kenya, vinara wa uchaguzi huo mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti, 2022 wameendelea kutambiana majukwaani na kutoa kauli za kujinadi kila mmoja akivutia upande wake kwa kumtaja Uhuru Kenyatta kwa namna yake.
Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga ameahidi kuendeleza uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta akichaguliwa rais mwezi Agosti wakati wa mkutano wake Thika.
Akihutubia wafuasi katika uwanja wa Thika Jumamosi Januari 15, amesema atahakiksiha miradi yote iliyoanzishwa na Rais imeendelea huku akiwaambia wafuasi wake kuwa yeye ndiye alikuwa mwazilishi wa ujenzi wa barabara katika eneo la Mt Kenya.
“Thika SuperHighway mimi ndio nilijenga mpaka ikafika hapa, hata hii kutoka Kenol hadi Marwa ilichorwa wakati wangu. Na sasa Uhuru amejenga, na sasa kuna barabara nyingi zinajengwa, na ninataka nihakikishie nyinyi ile miradi yote inaendelea nitahakikisha nimemaliza,” alisema Raila.
Aliahidi wakazi pia kuwa serikali yake itahakikisha kila mwanafunzi anasoma hadi chuo kikuu bila kutozwa karo. “Nitawafunga Kamiti,” akiahidi kuwafunga viongozi Fisadi, Kila mtoto ambaye amezaliwa katika taifa letu hata kama wazazi hawana pesa atapata nafasi sawa katika nasari, shule ya msingi, sekondari na chuo kikuu, na kisha apate kazi ya maana si wheelbarrow,” alisema Raila.
Raila alichukua nafasi hiyo kumlima kisiasa naibu rais William Ruto, akisema ameshindwa na kazi tangu aingie mamlakani.
“Umekuwa serikalini kwa miaka minane lakini umefeli. Wacha Baba akufunze namna ya kufanya kazi. Mimi nimekuwa kwa serikali na ninajua mahali pesa iko. Kila jamii ambayo haijiwezi itakuwa inapata KSh 6K,” alisema.
Alisema DP Ruto alishindwa kutimiza ahadi alizoahidi pamoja na Rais Uhuru Kenyatta walipokuwa wakiomba kura. “Aliahidi stadium, mumeona stadium hapa Thika? Na akaahidi tarakilishi kwa watoto lakini sasa ameanza kupeana wheelbarrow,” alisema Baba.
Upande wa Kiongozi wa Chama cha Mashinani Isaac Ruto, amesimulia vile Rais Uhuru Kenyatta alimpigia simu akimtaka asiunge mkono hatua ya Raila Odinga kuenda kujiapisha mwaka 2017.
Ruto alisema Rais alimpigia simu mara nne ambapo alimtaka kutokubali kushiriki zoezi hilo lililokuwa likipangwa na muungano wa NASA.
Alisema, “Rais Kenyatta alinipigia simu na kuniambia hatufai kutumbukiza nchi katika mzozo wa kisiasa. Tuliongea mara nne, na akaniuliza ni gani muhimu kulalamikia vile uchaguzi ulifanyika au kuhakikisha nchi haijatumbukia kwenye mzozo wa kisiasa.”
Alisema Rais alichangia pakubwa uamuzi wake wa kugura muungano na NASA na kujiunga na Jubilee. Wakati huo Ruto alikuwa amepoteza kiti cha ugavana kwa Mama Joyce Laboso wa Jubilee lakini akaamua kuweka hilo kando na kuunga mkono Rais.
Mwanasiasa huyo alifichua pia kuwa NASA ilikuwa na mgawanyiko kwani si wote waliokuwa wakiunga mkono Raila kuapishwa na alifichua kuwa atawania kiti cha ugavana akisema anahofia mtu anaweza kukoroga mchujo wa UDA.
“Kama ningeenda Jubilee, singeponea mchujo wa Jubilee. Ni hivyo tu iwapo nitaingia UDA leo. Mtu anaweza kuhitilafiana na mchujo wa chama hicho,” alisema Ruto.
Hata hivyo, alisema anamuunga mkono naibu rais William Ruto kuwania urais katika uchaguzi wa Agosti mwaka huu. Ruto wamekuwa na uhasama wa kisiasa na DP kwa muda sasa huku ushindani wa siasa za Bonde la Ufa ukichacha.