Beki na nahodha wa Man City Vincent Kompany atakosa mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya AS Monaco utakaopigwa baadae hii leo kwenye uwanja wa Etihad Stadium.
Meneja wa Man City Pep Guardiola, amethibitisha taarifa za kutokuwepo kwa beki huyo katika mpambano wa leo ambao utashuhudia Man City wakisaka nafasi ya kutinga kwenye hatua ya robo fainali.
Guardiola aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano maalum kuelekea kwenye mpambano wa mkondo wa kwanza wa 16 bora wa ligi ya mabingwa barani Ulaya, Kompany bado anasumbuliwa na maumivu ya mguu aliyoyapata mwishoni mwa juma lililopita.
Alisema wakati wa maandalizi ya mchezo wa kombe la FA dhidi ya Huddersfield Town uliomalizika kwa sare ya bila kufungana, beki huyo kutoka nchini Ubelgiji alipata maumivu ya mguu.
Hata hivyo Guardiola aliwaeleza waandishi wa habari matarajio ya kumtumia Kompany kwenye mchezo wa marudio wa kombe la FA dhidi ya Huddersfield Town utakaochezwa Februari 28 kwenye uwanja wa Etihad Stadium.
Katika hatua nyingine meneja huyo kutoka nchini Hispania, alisema huenda akamuanzisha katika kikosi cha kwanza beki wa pembeni Gael Clichy ambaye alikua anasumbuliwa na maumivu ya mgongo.
Kuhusu nani atakaa langoni mwa Man City katika mpambano wa leo kati ya Claudio Bravo ama Willy Caballero, Guardiola alisema maamuzi hayo atayafanya muda mchache kabla ya mpambano kuanza.