Klabu ya AC Milan imemaliza hali ya sintofahamu, kwa kumtangaza Vincenzo Montella kama mkuu wa benchi la ufundi kuanzia msimu ujao wa ligi.

Montella mwenye umri wa miaka 42, ametangazwa kuchukua nafasi hiyo baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili ambao una masharti ya kuhakikisha AC Milan inarejea katika makali yake.

Montela ambaye amewahi kuzifundisha klabu kadhaa za nchini Italia, amechukua nafasi Cristian Brocchi, aliyetangazwa kuwa mkuu wa benchi la ufundi kwa muda majuma kadhaa kabla ya kumalizika kwa msimu wa 2015-16 akiziba nafasi iliyoachwa wazi na Sinisa Mihajlovic.

“Vincenzo Montella ndiye meneja wetu mpya, amekubali kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia klabu yetu na ataanza kazi rasmi  Julai 1,”

“Tunaamini uwezo na uzoefu wake katika ligi ya Sirie A, utasaidia kufanikisha kuiona AC Milan mpya itakayorejea katika ushindani.

“Pia tunamshukuru Cristian Brocchi kwa kukubali kuwa nasi katika sehemu ya mwisho ya msimu uliopita, tunathamini na kutambua mchango wake mkubwa ambao ulituwezesha kumaliza katika nafasi ya saba msimu uliopita.” ilieleza taarifa iliyochapishwa katika tovuti ya klabu ya AC Milan.

Msimu uliopita Montella, alikiongoza kikosi cha Sampdoria akiwa kama mbadala wa Walter Zenga aliyeondoka klabuni hapo na alikuwa chaguo la kwanza la AC Milan kabla ya kuajiriwa kwa Mihajlovic.

Klabu nyingine zilizowahi kutumikiwa na Montella ni AS Roma (2011), Catania (2011–2012), Fiorentina (2012–2015) pamoja na Sampdoria (2015–2016).

Real Madrid Wapanga Kuitega Juventus
England Kuachana Na Makocha Wazawa