Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Brazil na klabu ya Real Madrid ya Hispania, Vinicius Jr atakuwa nje ya dimba hadi Februari 2024 baada ya kuumia kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Colombia
Vinicius Jr alishindwa kuendelea na mchezo huo uliopigwa mwishoni mwa juma lililopita na kutolewa nje akiwa anachechemea, halia mbayo ilipelekea kuzusha hofu kwa Mashabiki wa Real Madrid.
Kabla ya kuumia Kiungo huyo alitengeneza nafasi ya bao lililowekwa kimiani na Gabriel Martinelli dakika ya nne lakini alishindwa kuendelea na mchezo kutokana jeraha alilopata, nafasi yake ilichukuliwa na Joao Pedro.
Vinicius Jr mwenye umri wa miaka 23 amekuwa akikabiliwa na tatizo la maumivu ya misuli ya paja msimu huu 2023/24, huku maumivu mengine sehemu ya paja yakibuka.
Baada ya mchezo kumalizika Vinicius alisema: “Jeraha hili linafanana na lile lililopita, nilikuwa na uvimbe ndio mana nikasikia maumivu. Nadhani ni ngumu (kucheza dhidi ya Argentina) kwa sababu madaktari walisema, tutafanya juu chini kuona kama kuna uwezekano.”
Sasa taarifa imethibitishwa Vinicius aliondolewa kwenye kikosi cha Brazil ambacho kinajianda na mchezo mwingine wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Argentina keshokutwa Jumatano (Novemba 22).
Kuumia kwa mchezaji huyo ni pigo kwa Real Madrid, kwani inakabiliwa na wachezaji wengi majeruhi wa kikosi cha kwanza na hivi karibuni kiungo wa timu hiyo Eduardo Camavinga aliumia akiwa katika majukumu ya kimataifa na timu ya taifa ya Ufaransa na taarifa imetolewa atakuwa nje ya dimba hadi Januari 2024.