Nyaraka za Pandora zimebainisha kuwa viongozi wapatao 35 ulimwenguni kote na mabilionea kadhaa wanamiliki kampuni au akaunti za benki za nje kukwepa kulipa kodi.
Uchunguzi huo umefanywa na Jumuiya ya Kimataifa ya Wanahabari wa Upelelezi (ICIJ) na timu ya vituo 150 vya habari – pamoja na idhaa ya Kituruki ya DW – umegundua kuwa watu mashuhuri wapatao 330 ulimwenguni kote wanamiliki akaunti kama hizo za siri za nje ya nchi.
Kwa upande wa Afrika, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na mama yake wametajwa kwenye nyaraka hizo kuwa wanamiliki akaunti za siri Panama. Aidha, ndugu zake watatu, wanamiliki kampuni tano za nje ya nchi zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 30. Kenyatta na familia yake hawakujibu maombi ya ICIJ ya kutoa maoni yao juu ya taarifa hizo.
Naye Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan ni miongoni mwa viongozi ambao wametajwa katika taarifa za siri zilizovuja ambazo zinaonyesha mali zinazomilikiwa kwa siri na viongozi hao.
Waraka huo wa taarifa za siri Pandora Papers unaonyesha kuwa Mfalme Abdullah wa Pili anamiliki mali za dola milioni mia moja za Kimarekani ambazo zimewekezwa kwa siri katika miji mbalimbali ikiwemo Malibu, California, Washington na London.
Viongozi wengine wanaotajwa katika waraka huo ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Czech – Andrej Babis ambaye anamiliki mali za thamani ya dola milioni 22 za Kimarekani ambazo zimewekezwa kwa siri Kusini mwa Ufaransa.