Viongozi waliochaguliwa wa Chama cha Muungano cha Azimio la Umoja One Kenya, wameidhinisha uamuzi wa uongozi wake kupinga katika Mahakama ya Juu tamko la mgombea Urais wa Kenya Kwanza, William Ruto kuwa Rais mteule.

Kiongozi wa Azimio na mgombea wa Urais katika uchaguzi wa Agosti 9, Raila Odinga walisema viongozi hao walikuwa wamefahamishwa kuhusu suala hilo na kisha wakaidhinisha hatua hiyo.

“Leo tulifanya mkutano wa kufahamiana na viongozi wetu waliochaguliwa kutoka kote nchini na tukazungumza juu ya njia ya kusonga mbele na tumewapa maelezo mafupi kuhusu uchaguzi wa urais na wameidhinisha,” amesema Odinga katika mkutano uliofanyika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta (KICC).

Mkutano huo uliwajumuisha Wabunge, Maseneta na Magavana waliochaguliwa chini ya bendera ya muungano wa Azimio, huku mgombea mwenza wa Odinga, Bi. Martha Karua akisema wana imani kuwa wataibuka washindi kufuatia mchakato wa kisheria wanaoufuata.

“Ushindi wetu umeahirishwa na unakuja nyumbani, huo ndio ujumbe wetu,” Bi Karua alisema huku Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka akidai mapambano bado yanaendelea na kwamba wana imani kuwa ushindi utakuwa upande wao.

“Hatua yetu ya kukataa matokeo ya uchaguzi imevuta hisia za wengi ulimwengu na tuko tayari kuhakikisha nchi haipati mkosi,” aliongeza Musyoka.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati Agosti 15, 2022 alimtangaza William Ruto kuwa rais mteule baada ya kupata kura 7,176,141 (sawa na asilimia 50.49) na kufikisha kiwango kilichohitajika.

Ili kushinda uchaguzi huo, ilitakiwa mmoja wa wagombea apate asilimia 50 pamoja na kura moja inayohitajika katika duru ya kwanza, ambapo Ruto alimshinda Odinga ambaye alipata asilimia 48.85 ya kura.

Kenya: Raila akataa matokeo ya urais, asema hatakubali

Uganda yalazimika kununua umeme Kenya
Anusurika kifo kwa kujichinja kisa ugumu wa maisha