Marekani imesema kuwa iko pamoja na wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kufuatia zoezi la kihistoria la kukabidhiana madaraka kwa amani, huku ikitangaza kuwapiga marufuku kuingia Marekani baadhi ya viongozi kutoka tume huru ya uchaguzi (INEC), serikali na jeshi la nchi hiyo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo ambapo ameweka wazi kwamba kutokana na kujihusisha katika ufisadi mkubwa unaohusiana na mchakato wa uchaguzi.

Ametaja orodha ya viongozi ambao hawatakiwi kuingia nchini Marekani kuwa ni Corneille Nangaa, Mwenyekiti wa Tume huru ya uchaguzi (CENI) ya DRC, Norbert Basengezi Katintima, Makamu mwenyekiti wa CENI, Marcellin Mukolo Basengezi, Mshauri wa Mwenyekiti wa CENI, Aubin Minaku Ndjalandjoko, Spika wa Bunge la Taifa la DRC, na Benoit Lwamba Bindu, Rais wa Mahakama ya Katiba DRC, na familia zao za karibu hawaruhusiwi kuingia nchini Marekani.

Taarifa ya wizara hiyo imesema kuwa Kifungu 7031 cha Sheria ya Wizara ya Mambo ya Nje, operesheni za nje ya nchi imempa madaraka wakati wowote Waziri wa Mambo ya Nje akiwa na taarifa za uhakika kuwa maafisa wa serikali za kigeni wamejihusisha na ufisadi mkubwa au kuvunja haki za binadamu, watu hao na familia zao wasiruhusiwe kuingia Marekani.

Aidha, taarifa hiyo ya wizara imesema kuwa watu hao wamejitajirisha kupitia ufisadi, wameamrisha au kusimamia uvunjifu wa amani dhidi ya raia, wakati wananchi hao walipokuwa wanatekeleza haki zao za kukusanyika kwa amani na uhuru wa kujielezea.

Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje imesisitiza kuwa hatua hiyo iliyotangazwa inaelekezwa kwa maafisa maalum na siyo kwa wananchi wa Congo au serikali mpya iliyoingia madarakani.

 

Majaliwa azitaka benki kupunguza riba za mikopo
Mbivu mbichi za Maalim Seif, Prof. Lipumba machi 17, Katakata ya umeme yaanza