Viongozi watatu wa nafasi za juu katika Mtandao wa wanafunzi Tanzania (TSNP) wameitikia wito wa kufika kwa upelelezi wa makosa ya Jinai (DCI) Jijini Dar es Salaam leo asubuhi kwa lengo la kuhojiwa kufuatia tukio la kutoonekana kwa Mahmud Abdul Omary Nondo aliyesemekana kutekwa huku taarifa za kiuchunguzi toka jeshi la polisi zikibainisha kuwa mwanafunzi huyo alikwenda kumtembelea mpenzi wake Iringa.
Taarifa hiyo imetolewa na Afisa Habari wa Mtandao wa Wanafunzi (TSNP), Hellen Sisya baada ya Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kuwataka viongozi hao kufika katika ofisi za DCI.
“Tumepokea taarifa ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inayotofautiana kabisa na ile ya Iringa juu ya kuonekana kwake” amesema Sisya.
”Hata hivyo, kabla ya taarifa ya uchunguzi kulitanguliwa na matamko ya viongozi wa juu waliodai kuwa Abdul Nondo alijiteka mwenyewe jambo ambalo kwa vyevyote lingeathiri uchunguzi wa jeshi la polisi“, amesema Hellen.
Pamoja na hayo, Hellen ameendelea kwa kusema “pamoja na mapungufu yote tunaamini Nondo atatendewa haki atakapofikishwa mahakamani”.