Katika kuhakikisha wanashinda mchezo wa Jumapili (April 16) dhidi ya Young Africans, baadhi ya viongozi Klabu ya Simba SC kutoka kamati mbalimbali wamehamishia shughuli zao kambini ili kujihakishia ushindi.
Kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, Young Africans na Simba zilitika sare ya bao 1-1. Na sasa Young Africans kileleni mwa ligi ikiwa na alama 68 mbele ya Simba wenye alama 60 tu.
Taarifa kutoka Simba SC zimeeleza kuwa, tangu kikosi hicho kimeingia kambini huko Mbweni baadhi ya viongozi wamekuwa wakishinda huko na kutoka usiku mnene ili kuhakikisha wanawatia moyo na nguvu wachezaji wao.
“Kiukweli tangu tuingie kambini kuna baadhi ya viongozi wamekuwa hawaishi mazoezini na kambini nadhani lengo ni kuendelea kutoa hamasa kwa ajili ya mechi yetu ijayo ambayo kila kiongozi anatutaka tuifunge Yanga,” zimeeleza taarifa hizo
Kwa upande wa Meneja Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema: “Ukubwa na umuhimu wa mchezo huu kwetu ni lazima tushikamane maana tunahitaji kuifunga Young Africans tu.”
“Hakuna kiongozi au Mwanasimba anayetaka kuwaona Young Africans wakitangaza ubingwa dhidi yetu, hivyo tumejipanga kuvuna ushindi bila kujali staili tutakayoitumia maana hatujawafunga muda na sasa heshima yetu pekee ni kuwapa kichapo.”