Uongozi wa klabu ya Simba jana Alhamis majira ya jioni ulivamia mazoezi ya timu yao yaliyokua yakiendelea katika viwanja vya Mo Simba Arena, Bunju jijini Dar es salaam.
Dhana kubwa ya Uongizi wa klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kufika katika viwanja hivyo, ilikua ni kuwatia ndimu wachezaji kuelekea mchezo wa Jumamosi (Julai 3) dhidi ya Young Africans.
Viongozi waliofika kushuhudia mazoezi hayo ya mwisho mwisho ni Zacharia Hanspope (Mwenyekiti Kamati ya Usajili), Mohamed Nassoro, Mtendaji Mkuu Barbara Gonzalez pamoja na Cresentius Magori.
Baada ya kufika uwanjani hapo viongozi hao, walisimama kwa dakika chache na kuzungumza na baadae kwenda katika jukwaa la uwanjani hapo kutizama mazoezi huku sura zao zikijaa furaha.
Wakati huo huo mashabiki walijitokeza kidogo uwanjani tofauti na ilivyozoeleka katika maandalizi ya Dabi nyingine huko nyuma.
Hata hivyo kujitokeza kwao kwa uchache hakumaanishi kama wameisusa timu yao pendwa, zaidi ya kuaminika kuwa huenda walikua kwenye maandalizi ya kuhakikisha wanakuwa sehemu ya mchezo wa kesho Jumamosi, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Simba SC inakwenda kwenye mchezo huo, ikiwa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 73, ikifuatiwa na mpinzani wake wa kesho Jumamosi Young Africans yenye alama 67 na Azam FC inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 64.