Scolastica Msewa, Kibaha – Pwani.
Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa – SUKI, Rabia Abdallah Hamid amewataka Viongozi Vijana wa Chama cha Mapinduzi – CCM, kuendeleza amani, maelewano na mshikamano uliopo kati ya Tanzania na Chama Kikomunisti cha China – CPC, kwa maslahi ya chama, jumuia zake pamoja na Maendeleo ya Nchi.
Rabia ametoa wito huo wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo Vijana 50 wa UWT na UVCCM katika masuala mbalimbali ya Uongozi wa Kisiasa yaliyowezeshwa na CPC Kibaha Mkoani, Pwani katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julias Nyerere, Kibaha kwa Mfipa.
Amesema, “CCM ina matarajio makubwa baada ya mafunzo hayo ya siku kumi kwamba utendaji na uongozi wa viongozi hao wa UVCCM na UWT utakuwa bora na wa mfano katika maeneo mbalimbali ya nchini yetu, nitoe rai kwenu kuendeleza roho ya amani, maelewano na mshikamano, pia kuwa sehemu ya kuchagiza mahusiano tuliyonayo na vyama rafiki ikiwemo CPC ,ikikumbukwa kwamba Umoja wetu ni nguvu.”
Naye Mkuu wa Shule hiyo ya Uongozi Prof. Marcelina Chijoliga amewashukuru CPC kwa kuwezesha mafunzo Vijana ambao wanaonekana wameiva katika kutumikia Chama, huku akiomba uongozi wa CPC kuendelea kufadhili Mafunzo ya kuwajengea uwezo wa uongozi kwa CCM na jumuia zake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Kimataifa – CPC, Yu Hailin amesema mafunzo hayo yamedumisha urafiki mkubwa na mahusiano kwa washiriki hai huku akiahidi kuwaalika nchini china Viongozi hao ili waweze kwenda kujifunza masuala mbalimbali ya kimaendeleo.
Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Shaban Mlao alisema makundi ya Vijana na wanawake ni tegemeo kubwa katika upatikanaji ushindi wa CCM na kuwataka Vijana hao kwenda kuwafundisha wenzao elimu waliyoipata katika Mafunzo hayo ya siku kumi.