Marekani imewawekea vikwazo viongozi wawili waandamizi wa kundi la kigaidi la Al-Shabab, waliohusika na utekelezaji wa shambulio la kigaidi, katika kambi ya jeshi la Marekani, nchini Kenya.
Wizara ya Mambo ya Nje Marekani, imesema kuwa imewatambua Abdullahi Osman Mohamed na Maalim Ayman katika orodha ya magaidi wa kimataifa.
Taarifa kutoka wizara hiyo imesema Mohamed ni mtaalamu mwandamizi wa vilipuzi wa kundi la Al-Shabab, na kiongozi wa masuala yao ya mawasiliano, huku Ayman akihusishwa na kupanga shambulizi lililotokea katika kambi ya Simba.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema raia nchini humo wamepigwa marufuku kujihusisha na shughuli za miamala za aina yoyote na Mohamed na Ayman, na mali zao nchini Marekani zimeshikiliwa.
Afisa mmoja wa jeshi la Marekani na wakandarasi wawili waliuawa mnamo mwezi Januari, kwenye shambulio lililtokea katika kambi ya Simba, kisiwa cha Manda.
Hilo lilikuwa shambulio la kwanza kutekelezwa na kundi la Al-Shabab dhidi ya jeshi la Marekani, nchini Kenya.