Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Songwe, Eliniko Mkola amewapiga marufuku viongozi wa Chama hicho Mkoani Songwe kutoa vitisho vya aina yoyote kwa Watumishi wa Serikali Mkoani humo.

Ameyasema hayo jana wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Songwe kilichoketi kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha Januari mpaka Juni 2019 ambapo taarifa hiyo ilipokelewa na kupitishwa.

“Liko tatizo la baadhi ya viongozi wa chama kusikiliza maneno na kutoyafanyia uchunguzi pia Wapo baadhi ya viongozi wa Chama hutishia viongozi wa Serikali, ni marufuku kwa vitendo hivyo kuanzia leo,” amesema Mkola.

Amesema kuwa taasisi zote zinafanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu hivyo ni vyema kujenga mazoea ya kuzisoma ili viongozi wa chama na wale wa serikai kila mmoja ajue mipaka yake ya utendaji kazi.

Mkola ametoa rai kwa viongozi wa chama na serikali kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuujenga Mkoa wa Songwe kwani wote wana nia moja ya kuhakikisha maendeleo yanapatikana Mkoani humo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela amesema kuwa viongozi wa serikali waliopo hawana nia ya kuuharibu Mkoa wa Songwe hivyo viongozi wa chama wawatumie katika kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.

Brig. Jen. Mwangela ameongeza kuwa endapo viongozi wa chama wataona kuna mambo kwenye Mkoa au Halmashauri zao hayaendi vizuri wawasilishe masuala hayo kwa viongozi walioko mkoani humo ili yafanyiwe kazi na pia wajitahidi kuepuka misuguano isiyo ya lazima.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, David Kafulila amesema kuwa viongozi wa chama na Serikali wasioneane aibu kuelezana ukweli kuhusu mapungufu ya baadhi ya watendaji wa serikali kwani kufanya hivyo maendeleo ya mkoa yatachelewa.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 31, 2019
Serikali yafuta miliki ya mashamba ya Mkomazi mkoani Tanga