Viongozi wa Dini Nchini wameaswa kuendelea kumuombea Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha wa chama cha mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni mlezi wa chama hicho katika mkoa wa Njombe Dkt. Frank Hawassi wakati akizungumza na Viongozi wa Dini wilaya za Ludewa, Makete, Wanging’ombe pamoja na wilaya ya Njombe mkoani humo.

”Viongozi wa Dini nchini mna jukumu kubwa la kuendelea kumuombea Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Taifa letu, naomba niwahakikishie ndugu zangu Watanzania kuwa Rais tuliyenaye ni mtu anayejali shida za Watanzania hasa wanyonge, najua ipo siri kubwa katika maombi, viongozi wa Dini mnalijua hili,’’ amesema Dkt. Hawassi.

Aidha, katika hatua nyingine Dkt. Hawassi amewataka wazee wote nchini kutumia hekima na busara zao walizojaliwa na mwenyezi mungu kukemea na kutoa ushauri juu ya mambo yasiyofaa ikiwemo kutoa ushauri kwa vijana nchini kuacha kufanya vitendo vya kulivunjia heshima Taifa badala yake vijana hao wawe chachu ya kukuza uchumi wa Taifa.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa chama cha mapinduzi CCM ngazi ya Taifa anatarajiwa kuhitimisha ziara yake ya siku sita katika mkoa wa Njombe baada ya kufanya vikao na wanachama katika wilaya zote za mkoa huo.

 

Makonda atoa milioni 5 msiba wa Godzilla
Wilaya ya Mufindi yaanza kuwabaini Wabakaji na Walawiti