Balozi wa Israel nchini Tanzania, Yahel Vilan ameipongeza Serikali kwa utendaji wake, amesema kuwa Serikali ya Israel itaimarisha kitengo cha wagongwa mahututi (ICU) katika hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa mkoani Dodoma pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wa kitengo hicho.
Pamoja na hayo, Balozi Vilan amesema viongozi wa makampuni 50 kutoka nchini Israel watakuja nchini mwaka huu kushiriki katika jukwaa la biashara na uchumi kati ya Tanzania na Israel, ambapo mbali na kushiriki katika jukwaa hilo, pia viongozi wa makampuni hayo watapata fursa ya kuangalia maeneo mbalimbali ya uwekezaji nchini.
Balozi Vilan amesema hayo leo Aprili 5, 2017 alipokutana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majliwa Ofisini kwake Bungeni mjini Dodoma.
Waziri Majaliwa amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Israel waje nchini kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo, ambapo amesema kuwa Tanzania na Israel ni nchini zenye uhusiano mzuri kwa muda mrefu, ambapo ameahidi kwamba Serikali itaendelea kuudumisha.
Aidha, Majaliwa amewakaribisha raia wa Israel kuitembelea Tanzania kama watalii kwa sababu kuna fursa nyingi za utalii ukiwemo mlima wa Kilimanjaro na mbuga nyingi zilizosheheni wanyama.