Kiongozi mwandamizi wa ngome ya umoja wa vyama vya upinzani ya National Super Alliance (NASA) nchini Kenya, Kalonzo Musyoka amedai kuwa Serikali imewaondoa walinzi binafsi waliokuwa wanawalinda viongozi wote waandamizi wa umoja huo.
Akizungumza muda mfupi uliopita nyumbani kwake jijini Nairobi, Musyoka amelaani kitendo hicho cha kuwaondolea walinzi binafsi (bodyguards).
“Kila aina ya ulinzi tumenyang’anywa. Lakini haya ni mapambano muhimu na bado tunaendelea kuzungumza. Vyombo vya habari vimeshambuliwa na sasa hata walinzi ambao tulikuwa tumepangiwa wameondolewa,” Musyoka anakaririwa na Citizen.
Aidha, amedai kuwa askari polisi waliokuwa wanalinda eneo la uwanja wa Uhuru Park ambao watu wamefurika kusubiri mpango wa kumuapisha Raila Odinga wameondolewa pia.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa NASA amewasihi wafuasi wao waliofika katika uwanja wa Uhuru Park kuendelea kuwa watulivu na kudumisha amani wakati viongozi wao wakiendelea kujadiliana hatua za kuchukua.