Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendeleza nidhamu katika matumizi ya fedha za umma, utekelezaji wa miradi ya kimkakati ukiwemo ujenzi wa reli ya kati, mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere lakini pia kuenzi lugha ya Kiswahili, kuwajali wananchi wanyonge na kudumisha umoja wa Kitaifa.

Ameyasema hayo leo Aprili 13, 2021 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022.

Waziri Mkuu pia ameainisha vipaumbele vya serikali katika kutekeleza mpango wa maendeleo kwa mwaka wa fedha 2021/22 mpaka mwaka 2025/26 kuwa ni pamoja na kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji na utoaji huduma, kukuza biashara, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu.

Ameongeza kuwa katika upande wa sekta binafsi kutokana na umuhimu wake katika ustawi wa kiuchumi na kijamii serikali kupitia mpango huo itahakikisha inaweka mazingira wezeshi.

Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya shilingi bilioni 116.8 kwa ajili ya Ofisi yake pamoja na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 ambapo kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 93.3 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 23.5 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Ajali yaua 10 Same, Rais Samia atuma salamu za rambirambi, atoa tahadhari
Serikali yanunua ndege mpya 3