Mkaguzi Kata wa Kata ya Ibaga, Mkaguzi msaidizi wa Polisi, Ibrahim Msangi amewaeleza waumini na jamii kiujumla kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inakataa uhalifu kama ambavyo Vitabu Vitakatifu, vinavyokataza uhalifu.
Msangi, ameyasema hayo wakati akitoa elimu ya ushirikishwaji jamii kwenye ufunguzi wa mkutano wa injili wa Kanisa la Kiinjiri la Kilutheri Tanzania – KKKT, Usharika wa Mkalama uliofanyika katika kiwanja cha soko la samaki, Kijiji na Kata ya Ibaga, Tarafa ya Kirumi, Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida.
Amesema, waumini na jamii inatakiwa kuuchukia uhalifu mara baada ya mafunzo hayo yanayolenga kujifunza matendo mema yenye kumpendeza Mungu, huku akitoa elimu juu ya namna ya kupambana na uhalifu kuanzia ngazi ya familia na mbinu salama za utoaji taarifa za wahalifu na uhalifu, kwa Jeshi la Polisi.
Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa hilo la KKKT, Joseph Makala amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kutoa elimu hiyo ambapo amesema limebadilika kwa kiasi kikubwa kwani hapo awali haikuwa rahisi Askari Polisi kuhudhuria Mikutano kama hiyo.