Kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23, Serikali ilitenga shilingi 42.5 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa kadi za Vitambulisho vya Taifa – NIDA, ambazo tayari zimeshalipwa na baadhi ya kadi zipo tayari huku nyingine zikiendelea kutengenezwa na kufikia mwishoni mwa 2023 wanaostahili watakuwa wameshavipata.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameyasema hayo jijini Mwanza wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluu Hassan aliposimama kuwasalimia wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa akiwa katika ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Mwanza.

Amesema, “Nachukua fursa hii kuwahakikishia Watanzania wote kwamba, changamoto ya Vitambulisho vya Taifa sasa inaenda kuisha, pamoja na kutenga fedha kwenye bajeti pia Rais, Mhe. Samia ameshatoa shilingi bilioni 28 za ziada kwa ajili ya kununua kadi kwa hiyo ifikapo mwezi Disemba, 2023, kadi zote zitakuwa zimekuja na Watanzania wote ambao wanastahili kadi hizo, watazipata kabla ya mwaka huu kuisha.”

Kuhusu suala la ulinzi na usalama, Masauni ametaja hatua ambazo Rais Samia amezichukua katika kuimarisha Jeshi la Polisi ikiwemo kutengwa kwa fedha shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kununua na kupeleka magari katika wilaya zote nchini ambapo miongoni mwa magari hayo, moja litaletwa katika Halmashauri ya Buchosa, pia baada ya kupeleka Askari katika Kata zote, sasa zinapelekwa pikipiki katika kata zote nchi nzima.

“Vilevile, ongezeko la bajeti ya wizara yetu kwa mwaka wa fedha 2023/24 kutoka shilingi bilioni 900 hadi trilioni 1.2 ni hatua kubwa ambapo kati ya fedha hizo, Mhe. Rais Samia ametuelekeza tupeleke mafuta moja kwa moja kwenye wilaya na kata zote nchini ili magari na pikipiki zilizosambazwa zifanye kazi ya kutoa huduma kwa wananchi bila changamoto yoyote kama ilivyokuwa zamani”, alieeza Masauni.

Aidha, ameongeza kuwa, kwenye bajeti ya mwaka 2023/24, Wizara imekuja na Mpango Kabambe wa kujenga Vituo vya Polisi katika kila Kata na amewaomba Wabunge na wananchi kushirikiana ili kutimiza malengo hayo kwa kuwa vitakapokuwa vimejengwa vituo katika kata zote, changamoto ya usalama katika maeneo mbalimbali nchini itaisha.

Romelu Lukaku anukia Saudi Arabia
Bajana azigonganisha Simba SC, Azam FC