Umoja wa Wamiliki wa Vituo Vya Mafuta Tanzania – TAPSOA, unafanya kila jitihada kuhakikisha vituo vya mafuta vinapata nishati hiyo bila kuchelewa, kutokana na foleni kubwa ya upakiaji wa mafuta kwenye maghala mbalimbali nchini.
TAPSOA wayasema hayo huku wakitoa shukrani kwa EWURA, Wizara ya Nishati na Taasisi nyingine za Serikali kwa kuweka utaratibu wa kupakia mafuta kwa masaa ya ziada, zikiwemo siku za Jumamosi na Jumapili, ili kupunguza msururu wa magari yaliyojazana kwenye maghala ya mafuta nchini.
“Wateja wetu katika vituo vya mafuta wasiwe na taharuki, jitihada zinaendelea na magari yanapakia mafuta, kutokana na jiografia pana ya nchi yetu, kwa baadhi ya maeneo huenda kukawa na ucheleweshwaji lakini magari yapo njiani kupeleka mafuta vituoni na kila eneo litapata mafuta,” wamebainisha TAPSOA.
Hata hivyo, Serikali imewapa maelekezo wenye maghala ya mafuta kufanya kazi saa 24 kwa lengo la kuhakikisha foleni za magari yaliyopo katika maghala zinapungua ili yawahi kupeleka mafuta vituoni na ikimbukwe kuwa Julai 23, 2023 wamiliki wa maghala ya Mafuta na waagizaji waliihakikishia serikali na Wananchi kuwamba wanayo mafuta ya kutosha.