Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watendaji wote Serikalini kuweka mkakati wa kudhibiti viashiria vyote vya uvunjifu wa amani katika maeneo yao.
Amesema hayo leo (Jumatano, Septemba 21, 2022) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani yayofanyika katika ukumbi ya Kuringe, Moshi Kilimanjaro na kusema lengo la agizo ni kuhakikisha nchi inakuwa katika hali ya utulivu, ili kufikisha maendeleo kila eneo.
Amesema, “Hatuna budi kuitunza amani yetu kulingana na umuhimu wake kwani amani ni tunda la upendo, utulivu, mshikamano na maridhiano. Serikali ya Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za kikanda na kimataifa katika kutafuta na kudumisha amani na usalama.”
Aidha ameongeza kuwa, “Jukumu la kudumisha amani na kuilinda amani ni ajenda ya kidunia inayomgusa kila mmoja, ili kulinda ustawi wa vizazi vya leo na kesho.” na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua na tahadhari ili kuendelea kudumisha amani nchini.
“Serikali ya Awamu ya Sita, inafanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha amani na usalama vinadumishwa kwa kuweka mikakati mbalimbali ya maendeleo inayolenga kutokomeza umaskini. Umaskini ni chanzo kikubwa cha migogoro sehemu nyingi duniani kwa sababu watu wanagombania kufaidika na rasilimali chache zilizopo.” amesema Waziri Mkuu.
Ameongeza kuwa kila palipo na amani, shughuli za kiuchumi na kijamii hufanyika kwa ufanisi mkubwa na hivyo kuchochea maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi kwa ujumla na kuongeza kuwa, “Niwasihi wananchi kuendelea kutunza na kuilinda tunu ya amani tuliyojaliwa hapa nchini.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuendelea kuunga mkono ajenda mbalimbali za maendeleo nchini ili kuhakikisha umaskini haugawanyi jamii bali uwe chachu ya kutafuta njia bora ya kujinasua katika hali hiyo.
Naye, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania, Zlatan Milisic ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuwa kinara katika kudumisha amani katika nchi za Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla ambapo pia ametowa wito kwa jamii kutambua umuhimu wa mahusiano ya karibu kati ya amani na maendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema kuwa viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro wataendelea kusimamia utunzaji wa amani tuliyonayo kwani ni tunu muhimu tuliyojaliwa nchini.
“Sisi viongozi wa mkoa wa Kilimanjaro tutaendelea kushirikiana na taasisi zote zikiwemo za dini kwani uwepo wa amani ni msingi wa ustawi wa wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro na Tanzania kwa ujumla”.
Siku ya amani duniani, huadhimishwa kila kila mwaka Septemba 21.