Wakulima wa mahindi katika eneo la Nyiragongo, lililopo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wameingia katika majonzi baada ya mashamba yao kuharibiwa na viwavi jeshi walioshambulia mazao huku bei ya nafaka ikipanda.
Wadudu hao wameshambulia majani na mashina ya mimea ya mahindi, hivyo mazao kushindwa kukua au kufikia hatua ya kuchanua maua baada ya wadudu hao kudaiwa kutokuwa na majira maalum kwani hutokea wakati wa kiangazi au masika.
Hali hiyo imesababisha kupanda kwa mazai aina ya nafaka katika soko la Goma, ambapo bei ya mahindi imepanda kwa kiasi kikubwa kutokana na kushuka kwa uzalishaji uliosababishwa na viwavi jeshi.
Mfanyabiashara wa mazao, Georgette Nyabadé anasema kuwa gunia la mahindi lililokuwa likiuzwa kwa 30 au 35, sasa linauzwa kwa dola 75 au 80 za Marekani na kuathiri chakula hicho kikuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wadudu hao waharibifu wa mazao, hutanda katika maeneo ya kitropiki na ya joto na wanasimuliwa kuweza kuharibu mashamba yote kabla ya kuendelea na utafutaji wao wa chakula na kuleta matokeo mabaya ya kiuchumi.
Uvamizi huo wa viwavi jeshi umesababisha hofu ya kuwepo kwa tatizo la chakula katika eneo ambalo tayari limekumbwa na uharibifu na inatarajiwa kuwa huenda kukatokea baa la njaa.