Serikali nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeagiza watu kuondolewa kutoka mji wa Goma, baada ya kutokea mlipuko wa volcano katika Mlima Nyiragongo.
Waziri wa mawasiliano wa nchi hiyo, Patrick Muyaya aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba hatua za kuwahamisha zimeanza kutekelezwa.
Hata hivyo, kabla ya serikali kutoa agizo hilo, maelfu ya wananchi walikuwa walishaanza kukimbia makazi yao. Huduma ya umeme pia ilikatika katika maeneo mengi ya nchi hiyo. Baadhi yao walielekea kusini karibu na mpaka wa Rwanda.
Leo Jumapili, watu wapatao 3,000 wameukimbia mji huo ulio mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuelekea Rwanda.
Balozi wa Rwanda nchini Congo DR, Vincent Karega, aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa anawakaribisha watu hao wanaokimbia janga hilo.
“Mipaka iko wazi na majirani zetu wanakaribishwa kwa amani,” ameandika.
Afisa mmoja katika hifadhi ya taifa ya Virunga iliyopo eneo ambako volcano imelipuka, amesema hadi leo asubuhi ujiuji wa moto (lava) unaotiririka kutoka Mlima Nyiragongo umefika uwanja wa ndege wa mji wa Goma na hivyo hali inazidi kuwa mbaya.
Katika ripoti yao ya Mei 10, wataalamu wa Goma walitoa tahadhari za kuwepo kwa dalili za kulipuka kwa volkano na walipendekeza kufuatilia ishara hizo kwa makini.