Kikosi cha Bishara United Mara kesho Ijumaa Novemba 20, kitarejea kwenye mchakato wa kusaka alama tatu za Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kupisha kalenda ya FIFA kwa zaidi ya juma moja.

Biashara United Mara inarejea kwenye mshike mshike wa Ligi Kuu huku wakiwa kwenye nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo msimu huu 2020/21, nyuma ya Simba SC kwa kufikisha alama 17, huku Dodoma Jiji FC wakiwa katika nafasi ya 11 kwa kumiliki alama 12.

Timu hiyo yenye maskani yake makuu mjini Musoma mkoani Mara, itakua ugenini mjini Dodoma kwenye uwanja wa Jamhuri, ikipepetana na wenyeji Dodoma jiji FC.

Kufuatia umuhimu wa mchezo huo, kocha mkuu wa Biashara United Mara Francis Baraza, amesema kikosi chake kipo ‘fiti’ na tayari kuwakabili Dodoma Jiji FC.

Baraza amesema kikosi chake kimefanya maandalizi ya kutosha na hana shaka na mchezo wa kesho ambao anaamini utamalizika kwa matokeo ya furaha upande wao.

“Tunajua mchezo wa kesho utakua mgumu na wenye upinzani wa hali ya juu, lakini kwa maandalizi mazuri tuliofanya, sina shaka, ninaamini hitaji letu la alama tatu litatimia.” Amesema Baraza

Michezo mingine ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa kesho Ijumaa Novemba 20, ni kati ya Ruvu Shooting dhidi ya Mbeya City wakati Mtibwa Sugar watawafuata Ihefu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga.

Sirro awaita Lissu, Lema
Watu 7 wauawa katika maandamano Uganda