Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kurejea tena Novemba 20, mwaka huu baada ya kupisha Kalenda ya FIFA, huku timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ikitarajiwa kucheza dhidi ya Tunisia Novemba 13 na 17.

Novemba 20, itashuhudiwa timu mbalimbali zikishuka dimbani, lakini siku moja baadaye Simba itakuwa ugenini dhidi ya Coastal Union wakati KMC FC ikiikaribisha Azam FC kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Novemba 22, Young Africans itashuka uwanjani kuikaribisha Namungo FC ikiwa inajua matokeo ya Azam FC dhidi ya KMC, endapo ikishinda itakaa kileleni kama ‘Wanalambalamba’ hao watapoteza ama kutoka sare, vinginevyo itazidi kumfukuza ‘mwizi’ kimya kimya.

Baada ya michezo hiyo, Novemba 24 Simba itaelekea ugenini katika Uwanja wa Samora kuivaa Dodoma Jiji wakati kesho yake kukiwa na vita kali kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam, wakati wenyeji Azam FC watakapoikaribisha Young Africans.

Endapo Azam FC na Young Africans kila mmoja atashinda mchezo wake dhidi ya KMC na Namungo, mchezo huo utakaozikutanisha ndio utaamua timu itakayokaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

Azam FC imeendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa kumiliki alama 25, baada ya kushika dimbani mara 10, ikifuatiwa na Young Africans yenye alama 24 huku Simba wakifikisha alama 20.

KMC FC kuivutia kasi Namungo FC
Magori: Fraga ameikwamisha Simba SC