Papa Francis amesema alitarajia kufika mji wa Goma uliopo nchini DRC lakini hataweza kutokana na vita inayoendelea na kusema ziara yake itaangazia hali inayowapata binadamu kutokana na migogoro ya muda mrefu na unyonyaji wa utajiri wa madini wa nchi hiyo.
Papa (86), alitarajiwa kutua katika mji mkuu Kinshasa karibu saa tisa saa za alasiri hii leo na kukutana na Rais Felix Tshisekedi, ambapo pia atatoa hotuba kwa maafisa, wanadiplomasia na wawakilishi wa mashirika ya kiraia.
Siku ya Jumatano (Februari 1, 2023), ataongoza Misa na kukutana na wahanga wa ghasia kutoka eneo la mashariki mwa nchi, ambalo limekumbwa na mapigano ya mara kwa mara kati ya waasi wa kundi la M23 na wanajeshi wa serikali.
Akiwa ndani ya Ndege, Papa aliwaambia waandishi wa habari kwamba alitaka kwenda Goma lakini hataweza kwa sababu ya vita vinavyoendelea na pia akazungumzia kuhusu masaibu ya wahamiaji wa Kiafrika, wanaovuka jangwa ili kufika Ulaya.