Vyama saba vya upinzani vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, vimesema kuwa vimefikia makubaliano ya kumsimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi wa Urais utakaofanyika Disemba mwaka huu.
Vyama hivyo vimeeleza kufikia makubaliano baada ya kufanya vikao kadhaa nchini Afrika Kusini na vimesema vitamtangaza mgombea wao kabla ya Novemba 15.
Uchaguzi huo utakuwa wa kwanza utakaoshuhudiwa kuachiana madaraka kidemokrasia nchini humo, Rais Joseph Kabila atakapolazimika kuachia madaraka baada ya kumaliza vipindi vyake viwili.
Aliingia madarakani Januari 2001, siku kumi baada ya baba yake Laurent Kabila kuuawa kwa kupigwa risasi na mmoja kati ya walinzi wake. Kabila alichaguliwa tena kwa kura mwaka 2006 na baadaye alichaguliwa tena kwa awamu ya pili mwaka 2011. Alipaswa kuachia ngazi tangu mwaka 2016 lakini aliendelea kwa miaka miwili mingine kwa sababu ambazo alidai ni za kiusalama wa nchi kabla ya kuitisha uchaguzi mwingine.
Rais Kabila na chama tawala wamemchagua aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Emmanuel Ramazani Shadary kugombea urais.
Aidha, waliokuwa wanatajwa kuwa wagombea wakuu wa upinzani, Jean Pierre Bemba na Moise Katumbi walikataliwa kushiriki uchaguzi wa mwaka huu.
Wakati mchakato wa maandalizi ya uchaguzi ukiendelea, wafuasi wa vyama vya upinzani jana walifanya maandamano makubwa katika mji mkuu wa Kinshasa kupinga mpango wa kutumia mashine za mfumo wa kielektroniki wa kuhesabu kura ambazo wamedai zimeletwa kwa kusudi la kuchakachua matokeo.