Baadhi ya madiwani, watendaji na wenyeviti wa Serikali za mitaa kutoka Wilaya Tatu za Mkoa wa Dar es Salaam wameviomba vyama vya siasa kutoa fursa za uongozi kwa wanawake ili waongezeke katika nafasi za uongozi ngazi mbalimbali.
Ombi hilo limetolewa na viongozi hao katika maoni yao walipokuwa katika semina kuangalia usawa wa kijinsia katika nafasi mbalimbali za uongozi iliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).
Aidha, baadhi ya viongozi hao na watendaji wamesema kumekuwa na changamoto nyingi ndani ya vyama vya siasa ambazo zinaendelea kuwa vikwazo kwa wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi katika vyama anuai, hivyo kama zikiangaliwa zinaweza kuongeza hamasa kwa wanawake kupata nafasi za uongozi
Hata hivyo wamewataka wanawake kuendelea kujitokeza, kujiunga na vyama mbalimbali vya siasa pia kushiriki kugombea nafasi ili waweze kuonekana na kukwaa nafasi hizo.
“Mbali na Vyama vya siasa kutakiwa kuregeza masharti na kutoa fursa kwa kundi la wanawake, wao pia wanatakiwa kujitokeza kushiriki katika siasa na kugombea nafasi mbalimbali ili waonekane,” amesema mshiriki mmoja katika semina hiyo.
Kwa pamoja viongozi hao walikubaliana kuendelea kuwaunga mkono kundi hilo katika ushiriki wa siasa ili kujenga usawa wa kijinsia katika nafasi za maamuzi kuanzia ngazi za chini na kuendelea.
Kwa upande wake Afisa Programu na Uchambuzi wa TGNP, Deogratius Temba akiwasilisha mada katika semina hiyo amesema kuwa wanawake ni wadau muhimu katika shughuli zote za kisiasa na maendeleo ya jamii hivyo kuna kila sababu ya kupewa nafasi ili waingie katika vyombo vya maamuzi.