Kufuatia kukamatwa kwa mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS), vyama vitatu vya wanasheria Afrika vimetoa tamko la pamoja kukosoa hatua hiyo.
Lissu alikamatwa na jeshi la polisi akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere alipokuwa anaelekea kwenye mkutano wa wanasheria wa Afrika Mashariki uliofanyika jijini Kigali nchini Rwanda.
Vyama hivyo vilivyotoa tamko la pamoja ni Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS), Chama cha Wanasheria cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-LA) na Muungano wa Wanasheria Afrika (PALU).
Katika tamko lao hilo, wamesema kuwa wataweka utaratibu wa kuanza kufuatilia mashtaka dhidi ya Lissu, huku wakibainisha kuwa kwakuwa suala hilo liko mahakamani hawatazungumza mengi.
- Polisi: Lissu hatoki Ng’o, mpaka upelelezi ukamilike
- Video: Vanessa aikumbuka B’Hitz ya Hammy B, mpango wa kuwa na watoto, ‘ya kisela’ na Jux
Vyama hivyo vimedai kuwa Lissu alikamatwa kabla ya kukamilika kwa uchunguzi wa tuhuma dhidi yake, kitendo ambacho wamedai ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria nyingine za kimataifa.
Tamko hilo limesainiwa na rais wa PALU, Elijah Banda, Rais wa SADC-LA, James Banda, na Rais wa EALS, Richard Mugisha.
Lissu ameendelea kushikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za uchochezi na nyumba yake imepekuliwa.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Lucas Mkondya alisema kuwa jeshi hilo halitamuachia Lissu hadi litakapokamilisha upelelezi na kisha kumfikisha mahakamani.