Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Khamis Hamza ametoa jumla vyeti 190 vya Tathmini ya athari kwa Mazingira, kwa ajili ya miradi mbalimbali katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2023.
Hamza ameyasema hayo wakati akiwasilisha Taarifa kuhusu Tathmini za Mazingira Kimkakati pamoja na ufanisi wa Tathmini za athari kwa Mazingira – TAM, kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira hii leo, Jijini Dodoma.
Amesema, “hatua hii inaunga mkono azma ya Serikali kuelekea uchumi wa viwanda hivyo Ofisi imeendelea kupokea miradi mingi kutokana na ongezeko la wawekezaji katika sehemu mbalimbali.
Hata hivyo, amesema ofisi hiyo imechukua hatua mbalimbali na kuweka mipango ya utekelezaji kwa kupunguza muda wa mchakato wa TAM, ambapo miradi hiyo huhitaji kupata cheti kilichosainiwa na Waziri mwenye dhamana ya Mazingira.
’’kupitia muongozo huu wa kanuni mpya kwa miradi yenye ulazima wa kupitia tathmini ya athari kwa mazingira muda umepungua na kufikia siku 95 kutoka 149 kama ilivyokuwa awali,”amesema.
Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa, “ili kuleta maendeleo endelevu, suala la uhifadhi wa mazingira halina budi kupewa kipaumbele na ili kuhakikisha ufanisi wa miradi ni vyema kuhuisha masuala ya mazingira katika shughuli za maendeleo hususan ufanyaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira.”