Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Philip Mpango amesema Serikali inathamini mchango wa vyombo vya habari katika kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili duniani na kuifanya lugha hiyo kuwa yenye hadhi.
Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Pili la Idhaa za Kiswahili Duniani Machi 14, 2022, Katika Ukumbi wa AICC Jijini Arusha.
Amesema lugha ya Kiswahili imekuwa bidhaa adhimu, watanzania, waandishi wa habari, watangazaji wanawajibu wa kuifanya lugha hiyo kuwa ya kwanza duniani ambayo inawazungumzaji wengi ikizingatiwa penye nia pana njia.
“Serikali ya Awamu ya Sita, inaunga mkono jitihada za kukiendeleza Kiswahili. Itakumbukwa kuwa toka tulipoingia madarakani kwa mara ya kwanza mwezi Machi 2021, kumekuwa na viashirio vingi vinavyoonyesha namna Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hasaan inavyounga mkono jitihada za kukiendeleza Kiswahili” Amesema Makamu wa Rais Dkt. Mpango.
Aidha, katika kuhakikisha lugha ya Kiswahili inaendelea kukua duniani, Dkt. Mpango amesema kuwa Serikali itaendelea kufundisha lugha ya Kiswahili kupitia Balozi mbalimbali za Tanzania duniani, huku akitoa wito kwa vijana kwa kuwahimiza kusoma na kuandika vitabu na majarida ya kiswahili yatakayowafikia watu wote.
Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa amesema lugha ya Kiswahili inaenea na kuenezwa haraka hususan kimataifa kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia na utashi wa watu wa mataifa mbalimbali wa kutaka kujifunza Kiswahili.
Amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la vyombo vya habari ambavyo vinatumia lugha ya Kiswahili hapa nchini ambavyo idadi yake ni 172 na duniani idadi yake ni 36 ambapo baahi yao wamefika kwenye Kongamano hilo kwa kuwa ni jambo jema wanahabari kukutana, kupata elimu kuhusu lugha na kujadili kwa pamoja mambo yanayowahusu na kufahamishana fursa mbalimbali zinazopatikana duniani kwa kupitia tasnia ya habari na Kiswahili.
Kongamano la Pili la Idhaa za Kiswahili Dunia linaongozwa na kaulimbiu inayosema “Tasnia ya Habari kwa Maendeleo ya Kiswahili Duniani” likitanguliwa na kongamano la kwanza lilifanyika Novemba 12-15, 2007 likiongozwa kwa lengo la kuimarisha uhusiano na vyombo vya habari ambavyo vinatekeleza jukumu la kukieneza Kiswahili duniani kwa kukitumia na kutangaza katika vituo vyao vya habari.