Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amevitaka vyombo ya habari vya Nchi za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania kutangaza na kuandika habari za kweli ili kujitofautisha na vyombo vya Nje ya Bara hilo ambavyo upotosha na kubeza kwa makusudi mambo mazuri yanayotekelezwa na yaliyotekelezwa na Nchi za Afrika.

Ameyasema hayo jijiini Dar es salaam katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Mawasiliano Barani Afrika, ambapo amesema kuwa vyombo vya Habari vya Afrika havina budi kuonyesha udhubuti kwa kuweka sera zinazoakisi maendeleo na kuyatangaza kwa Wananchi wake na wote waliopo nje ya Bara hilo.

Amesema kuwa sehemu kubwa ya maudhui ya Vyombo vya Habari vilivyopo nje ya Bara la Afrika vinavyoongozwa na Wakoloni waliowahi kutawala katika Bara la Afrika hawapendi kuona Nchi za Afrika zinapiga hatua za Maendeleo kwa wananchi wake na badala yake hupenda kuripoti na kutangaza mambo mabaya yanayohusu Afrika ikiwemo njaa, magonjwa, vurugu za kisiasa, vita n.k.

“Wakati Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Kenneth Kaunda wa Zambia walipoamua kujenga Reli ya Tazara, walipingwa vikali sana na Wakoloni waliotutawala na wengine waliita reli ile kuwa ni bamboo (mianzi) lakini ni taifa moja tu la Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China walitusaidia na leo hii reli ile ndiyo ndefu zaidi katika Bara la Afrika yenye urefu wa kilometa 1860,”amsema Dkt. Mwakyembe.

Kwa mujibu wa Waziri Mwakyembe amesema kuwa Maendeleo ya Bara la Afrika yatatetewa na kupiganiwa na Waafrika wenyewe, hivyo ni wajibu wa vyombo vya habari vya Bara hilo kujitokeza na kutetea Maendeleo hayo na kamwe haitatokea siku moja chombo cha habari cha BBC au CNN vikatangaza mafanikio hayo kwani hawapendi kuona Mataifa waliyoyatawala yakifikia hatua kubwa za kimaendeleo.

Akifafanua zaidi Dkt. Mwakyembe amewataka Vijana wa Nchi za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania kujifunza historia ya Bara lao ili kuweza kufahamu wapi walipotoka na wapi wanapoelekea badala ya kupenda kulalamika pasipo na kuweka mikakati ya namna bora ya kupiga hatua za kujietea Maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, amesema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za mawasiliano katika sekta binafsi ili kuhakikisha kuwa wanajenga daraja moja katika kusukuma mbele gurudumu la Maendeleo ya sekta ya habari na Mawasiliano nchini.

Naye Rais wa Chama cha Maafisa Uhusiano wa Sekta binafsi Tanzania (PRST), Loth Makuza amesema, taasisi hiyo ni jukwaa huru linalotoa fursa na nafasi ya kujadili masuala mbalimbali ya mawasiliano nchini ikiwemo changamoto na utatuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya habari na mawasiliano nchini.

Simba yafanya maandalizi ya kukabidhiwa kombe
RC Kagera aagiza Kaya zote na Taasisi kujenga Vyoo