Kambi ya Maalim Seif Sharif Hamad imeanza kupata nafasi za uongozi ndani ya chama cha ACT-Wazalendo, ikiwa ni takribani siku nane tangu wajiunge na chama hicho.
Leo, Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe amemtaja Juma Haji Duni kuwa ndiye Naibu Kiongozi na kwamba anaanza kazi yake kesho, Machi 27.
Hicho ni cheo cha pili kutoka juu ndani ya chama hicho, ambapo Haji atakuwa juu ya nafasi ya Mwenyekiti wa chama iliyoachwa wazi miaka miwili iliyopita na Mama Anna Mghwira ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
“Nimepewa mamlaka na Katiba ya chama kumteua, nikawasilisha kwa uongozi na wameridhia na ataanza kesho kutumikia nafasi hiyo,” Zitto aliwaambia waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Mwaka 2015, Juma Duni Haji alikuwa mgombea mwenza wa nafasi ya Urais kwa tiketi ya Chadema, akitokea CUF kwa makubaliano ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), lakini alirejea tena CUF baada ya uchaguzi mkuu, CCM iliposhinda nafasi hiyo.
‘Babu Duni alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF na alikuwa mmoja kati ya wanasiasa wenye ushawishi mkubwa ndani ya chama hicho.
Hatua ya kupewa nafasi hiyo ndani ya ACT-Wazalendo imekuja ikiwa ni siku chache tangu Maalim Seif aweke wazi kuwa walipoamua kujiunga na chama hicho hawakuweka masharti yoyote ya kupewa nafasi za uongozi.