Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Masha Mshomba amewataka waajiri wote Tanzania Bara kuwasilisha taarifa ya mapato ya wafanyakazi wao (Return of Annual Earnings) kwa kipindi cha mwaka mmoja, kuanzia tarehe 01.03.2016 mpaka tarehe 28.02.2017.
Amesema kuwa uwasilishwaji wa taarifa hizo ni kwa mujibu wa vifungu vya 73 (1) na 73 (2) vya sheria ya fidia kwa wafanyakazi sura ya 263 marejeo ya mwaka 2015 kinachomtaka kila mwajiri kuwasilisha taarifa hizo kabla ya tarehe 31 ya mwezi Machi kila mwaka.
“Nawataarifu waajiri wote kuwa uwasilishwaji wa fomu hizo ni kwa kutumia fomu WCR-3 na mwisho wa kuziwasilisha ni tarehe 31.03.2017,”amesema Mshomba.
Aidha, ameongeza kuwa fomu zilizojazwa kikamilifu ziwasilishwe kwenye ofisi za Mfuko zilizopo Jengo la GEPF House, Kitalu na 37, Regent Estate, Barabara ya Bagamoyo au Ofisi za Kazi zilizopo mikoani na wilayani kwa upande wa Tanzania Bara.
Hata hivyo, amesema, fomu WCR-3 inapatikana kwenye tovuti ya Mfuko huo www.wcf.go.tz, Makao Makuu ya Mfuko au kwenye Ofisi za Kazi zilizopo mikoani na wilayani.