Baadhi ya Waalimu wa shule za msingi kwenye Halmashauri ya mji wa Bunda, mkoani Mara wamekimbia vituo vyao vya kazi wakati wa mchakato wa uhakiki vya vyeti na kushindwa kuhakikiwa.
Kufutia hali hiyo Waalimu wakuu wa shule ambazo waalimu wao walitoroka, wametakiwa kuandika majina na taarifa sahihi juu ya waalimu hao ili waweze kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Janeth Peter Mayanja, wakati wa kikao cha kazi kilichoitishwa na uongozi wa Halmashauri ya mji huo kwa ajili ya kuwapongeza waalimu wa shule kumi za msingi zilizofanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana.
Mayanja amesema kuwa kuna baadhi ya waalimu wa shule za msingi katika Halmashauri ya mji huo wakati wa uhakiki wa vyeti walitoroka kwenye vituo vyao vya kazi na kwamba waalimu hao wasidhani kwamba uhakiki huo umeisha.
“Hiyo taarifa mnayo mnaijua baadhi yenu wakati wa uhakiki wa vyeti walitoroka na sasa wamekwisha rejea, wanadhani kwamba uhakiki umekwisha,”amesema Mayanja.
Aidha amesema kuwa waalimu wakuu wa shule hizo sasa wanapaswa kuandika taarifa sahihi juu ya waalimu waliokuwa wametoroka na sasa wamerejea.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji huo, Mayaya Magesse amewataka waalimu kufanya kazi kwa kufuata maadili ya utumishi wa umma,ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi na kwa wakati sahihi.