Hatimaye Kamati ya Waamuzi ya Shiriskisho la Soka Tanzania ‘TFF’ imejitokeza hadharani na kuanika ripoti ya utendaji kazi kwa waamuzi waliochezesha michezo ya mzunguuko wa 16 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mzunguuko wa 16 wa Ligi hiyo ulikwisha rasmi jana Ijumaa (Machi 04) kwa mchezo mmoja kuchezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo Mabingwa watetezi Simba SC waliikaribisha Biashara United Mara.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Nassor Hamdoun, amesema Mzunguuko wa 16 wa Ligi Kuu Tanzania Bara haukuwa na ‘kelele’ za wadau wa soka nchini kuhusiana na waamuzi kutokana na kamati yake kujitathnmini na kutoa maagizo sahihi yanayozingatia kanuni na taratibu kwa waamuzi walipopewa jukumu la kuchezesha.
Hamdoun amesema kwa sasa waamuzi wameongeza umakini kwa sababu wanafahamu wanahitaji kupata Bingwa wa ligi ambaye amepata ushindi wa halali na hiyo itapunguza malalamiko.
“Ni kweli tumemaliza raundi ya 16 na kuendelea bila malalamiko, tunashukuru na lazima tupongezane. Ni kwa sababu tumejitathmini, katikati ya ligi waamuzi huwa tuna semina kwa ajili ya kuangalia changamoto zilizojitokeza katika mzunguko wa kwanza ili zirekebishwe, na yale mazuri tuyashikilie,” amesema Hamdoun.
Kuhusu michezo inayofuata, kiongozi huyo amesema kuwa matumaini yake ni kuendelea na kuifanya Ligi Kuu Tanzania Bara iendelee kuwa bora kama ilivyo hivi sasa ambapo ni moja kati ya ligi 10 bora barani Afrika.
“Tunataka kuwafanya waamuzi wetu wawe wanachezesha kwa wingi nje ya nchi, na hatutasita kutoa adhabu pale tunapoona wanakwenda kinyume na inavyotakiwa.
Kuhusiana na malipo, Hamdoun, amesema waamuzi wa Tanzania ni moja kati ya wanaolipwa vizuri hapa barani Afrika, na sasa wanalipwa kwa wakati na kama hali ya ucheleweshaji itatokea, basi hutokana na sababu zisizozuilika.