Chama cha waamuzi wa soka mkoa wa Mwanza kimesitisha kutoa huduma ya uchezeshaji wa michezo ya ligi ngazi ya mkoa huo, baada ya kukosa maelewano na viongozi wa chama cha soka cha MZFA.
Mwenyekiti wa chama cha waamuzi wa soka mkoa wa Mwanza, Emmanuel Mataba amesema viongozi wa MZFA wameshindwa kufikiia makubaliano ya kuwalipa pesa waamuzi ambao walipaswa kuchezesha ligi ya mkoa.
Mateba amesema, MZFA wamekua wakiwazunguusha kuhusu malipo ya waamuzi ambayo wanayadai tangu mwaka 2016, na waliamini huenda ugeni wa viongozi walioingia madarakani ulikua kikwazo. Amesema wamekua wakifanya mazungumzo ya mara kwa mara, lakini hakuna maelewano mazuri kuhusu malipo yao, na wameona jambo sahihi kwa sasa ni kutangaza mgomo wa kutochezesha michezo ya ligi ya mkoa wa Mwanza.
“Tumezungumza na MZFA zaidi ya mara tatu kuhusu malipo yetu, tunadai zaidi ya shilingi milioni tatu (3,000,000), na walituahidi baada ya michezo wa Simba na Mbao FC, Simba na Toto Africans iliyochezwa hapa Mwanza mwezi huu, wangetulipa pesa zetu lakini imekua hadithi zisizoisha,”
“Tunaamini msimamo wa kugomea michezo ya ligi ya mkoa wa Mwanza itakua shinikizo zuri kwa viongozi wa MZFA ili wafanikishe mpango wa kutulipa pesa zetu, ambazo ni halali kwa kila mwamuzi aliyevuja jasho kwa dakika 90.” Amesema Mateba
Hata hivyo Mataba amesema cha kushangaza zaidi MZFA wamechukua jukumu la kuwatumia watu wengine ambao hawana taalum ya kuchezesha mchezo wa soka, na kuwapa majukumu ya kuchezesha ligi ya mkoa wa Mwanza.
“Kuvunjwa kwa utaratibu wa kuwatumia watu ambao hawana taalum ya uamuzi, tumekusudia kukata rufaa katika ngazi ya TFF ili kuonyesha mapungufu, ambayo yatazinyima haki timu zilizocheza chini ya usimamizi wa waamuzi feki.”
Dar24 imejaribu kumsaka katibu mkuu wa chama cha soka mkoa wa Mwanza (MZFA) Malongo Malongo tangu jana, ili kueleza tuhuma wanazotupiwa na chama cha waamuzi, lakini wakati wote simu ya kiongozi huyo imezimwa.