Waamuzi wa Tanzania waliochezesha mchezo wa ligi ya mabingwa barani Afrika kati ya LLB ACADEMIC ya Burundi dhidi ya RAYON SPORTS ya Rwanda wako hatarini kufungiwa na shirikisho la soka barani Afrika (CAF) kama watakutwa na hatia ya upangaji wa matokeo katika mchezo huo uliomalizika kwa RAYON SPORTS kushinda kwa 1-0 ugenini.
Shirikisho la Soka Tanzania TFF kupitia Kaimu Katibu Mkuu wake Wilfred Kidao limethibitisha waamuzi hao kufanyiwa uchunguzi na CAF, na kusema kuwa watakutana na kamati ya waamuzi baada ya siku mbili kuanzia leo ili kujadili ni nini kifanyike wakati wakisubiria hukumu kutoka CAF.
Kidao amesema kama waamuzi hao wakipatikana na hatia, waadhibiwe ipasavyo na kama wakiwa hawana hatia waachiwe huru.
Mfaume Ali Nasoro, Frank John Komba, Sudi Lila na Israel Mujuni ndiyo watuhumiwa kwenye tuhuma hizo na imeelezwa kuwa viongozi wa Rayon Sports walionekana kwenye moja ya chumba cha mwamuzi usiku wa kuamkia siku ya mchezo wenyewe, kitu ambacho kilizua tafrani kwenye hotel waliyokuwa wamefikia waamuzi hao na baadhi ya wageni (RAYON SPORTS) kukamatwa na polisi.
Msimamizi wa mchezo huo uliofanyika Februari 21 mwaka huu naye alikuwa katika hotel hiyo hiyo na kutokana na purukushani hizo alitoka nje na kuangalia hali ilivyokuwa inaenda ambapo aliandika ripoti yenye maelezo ya kilichotokea pamoja na ushahidi wa video za CCTV tayari kwa uchunguzi.