Mamia ya Wakenya, wameandamana katika mitaa ya jiji la Nairobi kuzitaka nchi tajiri kukabili mabadiliko ya hali ya hewa barani Afrika, kufuatia maeneo mengi ikiwemo Kenya kukumbwa na ukame mbaya zaidi katika kipindi cha miaka arobaini ambapo wengi wanalaumu juu ya ongezeko la joto duniani.
Mmoja wa wanaharakati mshiriki wa maandamano hayo, Duncan Omwami amesema mataifa yaliyoendelea kiviwanda yanapaswa kuwafidia kwa hasara waafrika walioathirika huku akiitaka Global North kulipia uharibifu uliotokea.
Amesema, “Kumbuka kutoka kwa ripoti ya IPCC, ya Jopo la Kiserikali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, ilisema asilimia 96 ya hewa chafu inatolewa na Global North sasa wanapaswa kutufidia.”
“Asilimia 4 inatolewa na Global South, Afrika kwa nafasi yetu ikiwa na asilimia 4 pekee, hatuna uwezo wa kutoa mchango wowote mkubwa katika uzalishaji huu kwa hivyo tunadai Global North ilipe hasara na uharibifu,” amesema Omwami.
Maandamano hayo, yalifanyika kama sehemu ya Muungano wa Haki za Hali ya Hewa wa Pan African huku vuguvugu hilo la maandamano ya mitaani likitaka mataifa tajiri kulipia uharibifu mkubwa uliofanywa katika ardhi ya wakulima wadogo na wafugaji, kote barani Afrika.
Elizabeth Wathuti, muandamanaji mwingine aliyeshiriki zoezi hilo anasema, “Majanga haya na changamoto hizi hazitokei Kenya pekee, zinatokea katika bara zima la Afrika na sisi bara letu limefanya uharibifu kidogo sana wa hali ya hewa lakini bado linaendelea kubeba mzigo mkubwa zaidi.”
Ameongeza kuwa, “Kwa hivyo, tunaomba kwamba nchi ambazo zimechangia zaidi katika mzozo huu hazipaswi kuachana na jamii hizi kwenye mstari wa mbele kwa hatima yao lakini zinapaswa kujitokeza na kutimiza ahadi walizotoa juu ya ufadhili wa hali ya hewa.”
Septemba 2021, karibu Wakenya milioni 3.5 waliathiriwa na hali mbaya ya hewa, huku serikali ikitangaza hali hiyo kuwa ni janga la kitaifa.