Maandamano ya wanaharakati wa mazingira yameibua mjadala katika mkutano wa Umoja wa Mataifa nchini Misri COP27, wakidai fidia ya uharibifu uliosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi kwa mataifa masikini Ulimwenguni.
Maandamano hayo ya Novemba 12, 2022 yamefanyika katika siku ya kimataifa ya utekelezaji wa haki za mazingira, wakati mkutano wa COP27 ukimalizika huku wajumbe wa mkutano huo wakiafikiana juu ya kuliweka suala la ufadhili kwenye ajenda, kwa mara ya kwanza.
Aidha, nchi zinazoendelea kwa muda mrefu zimekuwa zikishinikiza juu ya kuundwa kwa utaratibu wa kifedha, ili kushughulikia madhara yanayotokana na athari za kimazingira kwa nchi masikini Duniani.
Hata hivyo, Shirika la kimataifa la mazingira, Greenpeace, limesema nchi kadhaa zilizoendelea, zikiwemo Marekani na Uingerezaz zinazuia juhudi za kuundwa kwa kituo cha kushughulikia hasara na uharibifu katika mkutano wa COP27.