Vyombo vya usalama nchini Sudan vimetoa hati ya kukamatwa kwa waandishi wa habari 38 kwa tuhuma za uchochezi na kuandika habari za uongo mtandaoni.
Kwa mujibu wa Sudania24, hati hiyo ya kukamatwa imetolewa na kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jina pamoja na sheria ya makosa ya mtandaoni.
Mbali na waandishi hao, wanaharakati kadhaa ambao idadi yao haikutajwa na chombo hicho wako kwenye orodha ya wanaotakiwa kukamatwa.
Wanaharakati pamoja na waandishi wa habari nchini humo wamekuwa wakitumia zaidi mitandao ya kijamii kuripoti matukio yaliyokuwa yanaendelea katika maandamano ya kupinga kupanda kwa gharama za maisha. Waliweka video nyingi pamoja na picha za matukio.
Sudania24 imeeleza kuwa waandishi wa habari ambao ni raia wa Sudan lakini wako nje ya nchi pia ni miongoni mwa wanaotakiwa kukamatwa kutokana na tuhuma za uchochezi na kutoa habari za uongo.
Hatua hiyo ya Serikali imetangazwa ikiwa ni mwezi mmoja tangu yalipoanza maandamano nchini humo, ambapo pamoja na kupinga kupanda kwa gharama za bidhaa na huduma, waandamanaji wanataka Rais Omar al-Bashir kuondoka madarakani.
Juzi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alitoa wito kwa Serikali ya Sudan kuyasikiliza madai ya waandamanaji.
“Tunawaitaka Serikali ya Sudan kuwa sikivu kwa madai ya wananchi na kuheshimu haki za binadamu,” Guterres aliwaambia waandishi wa habari akiwa jijini New York nchini Marekani.
Al-Bashir ameiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha takribani miaka 30.