Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, SACP David Misime amewataka Waandishi wa Habari nchini kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kukuza maslahi ya Taifa pindi wanapotekeleza majukumu yao, huku Wadau wa Habari wakianisha changamoto mbalimbali zinzoikumba tasnia hiyo.
Misime ameyasema hayo wakati akifungua mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ulinzi na Usalama kwa Waandishi wa Habari ulioandaliwa na Umoja wa Vyama vya Waandishi wa Habari Tanzania – UTPC, wenye kauli mbiu isemayo “Shambulio lolote kwa Mwandishi wa Habari ni Shambulio kwa Umma.”
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi aliyefungua mdahalo huo, Mkurugenzi wa UTPC, Kenneth Simbaya alisema Mwandishi wa Habari anatakiwa kufanya kazi yake kwenye mazingira rafiki na bila kubughudhiwa, huku Mkurugenzi Mkuu wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben akisema asilimia 64 ya Wanawake waliopo katika Vyombo vya Habari vya Jiji la Dar es Salaama wamefanyiwa unyanyasaji wa Kingono.
Mbali na changamoto zinazoikabili tasnia ya habari nchini za taaluma hiyo kutokuwa na hadhi na heshima kama ilivyo kwa taaluma nyingine, ujira mdogo, kufanya kazi bila mikataba, changamoto nyingine ni pamoja na usalama wao pale wanapoibua mambo ndani ya mazingira yanayowazunguka, kusaka habari katika njia hatarishi, kutishiwa, kupigwa na kutekwa au kuuawa.