Waanzilishi wa Google, Larry Page na Sergey Brin wametangaza kujiondoa kwenye nafasi za Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) na Rais wa kampuni mama iitwayo Alphabet Inc.
Kampuni hiyo imetangaza uamuzi wa wawili hao Jumanne, Desemba 3, 2019 ikiwa ni miaka takribani 20 tangu walipoianzisha Google wakiwa pamoja.
Kutokana na uamuzi huo, CEO aliyepo hivi sasa wa Google, Sudar Pichai ambaye alikuwa kiongozi mwandamizi wa kampuni hiyo kwa muda mrefu ndiye atakayeyabeba majukumu yote yaliyoachwa na Larry na Sergey.
Hata hivyo, waanzilishi hao wataendelea kuihudumia kampuni ya Alphabet Inc. kama wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi.
“Hatujawahi kuchukua majukumu yote ya menejimenti wakati ambapo tuliona kuwa kuna njia bora zaidi ya kuendesha kampuni. Na sasa Alphabet na Google hazihitaji tena CEO wawili na Rais,” imeeleza barua yao ya pamoja.
Mabadiliko hayo ya kiutawala yamekuja wakati ambapo Google inakutana na changamoto kubwa ya kubanwa na wanasiasa na Mamlaka barani Ulaya na Marekani.
Mamlaka za maeneo hayo zimekuwa zikihoji ukubwa wa kampuni hiyo, uwezo wake wa kutunza faragha ya taarifa za wateja wake na madhara yake kwenye jamii.
Kwa mujibu wa CNN, Larry ambaye alikuwa anaonekana kama taswira ya kampuni hiyo, hivi karibuni alikuwa haonekani tena kwa umma akishindwa kuhudhuria hata mikutano mikubwa ya teknolojia aliyoalikwa.