Kiungo kutoka nchini Ufaransa na Klabu ya Juventus, Paul Pogba ameingia kwenye orodha ya mastaa wanaohitajika na matajiri wa Saudi Arabia katika dirisha hili la majira ya Kiangazi.
Pogba amekuwa na wakati mgumu Juventus tangu ajiunge na wababe hao wa Turin akitokea Manchester United katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana.
Taarifa zinaeleza kwamba Al Ittihad ya Saudi Arabia imeweka mezani ofa inayofikia mshahara wa Euro 100 milioni kwa mwaka ili kuhakikisha inampata Pogba ambaye mkataba wake na Juventus unamalizika 2026.
Hata hivyo, hadi sasa hakuna chanzo chochote kilicho karibu na Pogba kilichothibitisha suala hili na baadhi ya vyanzo vimedai hakuna ofa rasmi iliyowasilishwa kwa wawakilishi wa mchezaji huyu.
Ittihad ni miongoni mwa timu zilizosajili mastaa kadhaa wenye majina makubwa barani Ulaya ikiwa ni pamoja na N’Golo Kante kutoka Chelsea na Karim Benzema aliyeachana na Real Madrid.
Mambo yanazidi kupamba moto baada ya Pogba kuonekana Saudia, lakini hakuna uhakika wa asilimia mia ikiwa alikuwa huko kukamilisha dili au ishu zingine.