Kocha Mkuu wa Newcastle United, Eddie Howe amewapa presha makocha wenzake kwenye Ligi Kuu England baada ya kudai kwamba hajafuta mpango wa kuwanasa kwa mkopo mastaa wote wa maana waliopelekwa Saudi Arabia.
Saudi Arabia kupitia progamu yake maalumu chini ya Public Investment Fund ndiyo inayohusika na mchakato wa kununua mastaa wa maana na kuwapeleka kucheza soka kwenye ligi ya nchi hiyo, lakini pia ndio wamiliki wa asilimia 80 ya hisa za klabu ya Newcastle United.
Wakati kama N’Golo Kante, Ruben Neves, Roberto Firmino, Cristiano Ronaldo na Karim Benzema wamekwenda kukipiga huko Mashariki ya Kati, lakini timu walizokwenda kujiunga nazo zina uhusiano wa karibu kabisa na Newcastle, jambo ambalo linaweza kuwapa unafuu kama watahitaji saini zao kwa mkopo kwenye dirisha hili.
Kumbuka Newcastle United itacheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, hivyo jambo hilo linaweza kuwa kivutio kwa mastaa hao wakashawishika kurudi kwenye Ligi Kuu England kukipiga Ulaya, huku mishahara yao ikiendelea kuwa ile kwa maana ya kulipwa na klabu zao zilizowasajili huko Saudia.
Kocha Howe alisema: “Inategemea kama tukio iko sawa kwa Newcastle. Siku zote tunaangalia kilichobora kwetu.”
Akizungumzia mastaa wengi wa Ulaya kwenda Saudi Arabia, Howe alisema: “Sidhani kwamba ada ya uhamisho ni kubwa ni mishahara tu ndiyo inayovutia wachezaji.”
Kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, Newcastle United imemsajili kiungo Sandro Tonali kwa ada ya Pauni 55 milioni, huku kocha huyo akidai kwamba timu hiyo bado inahitaji wachezaji wenye viwango vikubwa kwa ajili ya msimu ujao.