Ni dhahir jina la Mshambuliaji wa Young Africans limekuwa sehemu ya maneno yanayotamkwa na USM Alger, baada ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Juzi Jumapili (Mei 28), Mshambuliaji huyo aliifungia Young Africans bao la kufutia machozi kwa umahiri mkubwa, huku USM Alger ikiambulia ushindi wa 2-1 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Mayele alifunga bao hilo dakika ya 82, linakuwa ni bao lake la saba kwenye Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu akiwa kinara.

Kocha Mkuu wa USM Alger, Abdulekh Banchikha, amesema kuwa walicheza na wapinzani wazuri ambao walikuwa wanapambana kutafuta ushindi wakiongozwa na Mayele.

“Umeona ulikuwa ni mchezo mgumu kwa pande zote, licha ya kwamba tulicheza mchezo mkubwa, bado mshambuliaji wao Mayele (Fiston) alifanya kazi nzuri na ni moja ya wachezaji wazuri.

“Niliwaambia wachezaji kuwa wanapaswa kucheza na timu kiujumla, lakini wasimuache mshambuliaji wao ambaye alitufunga, bado kuna mchezo wa pili nyumbani, hivyo kazi haijaisha kwa kuwa mpira una matokeo yake,” amesema Banchikha kabla ya kuanza safari ya kurejea nchini Algeria.

Katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa Fainali utakaochezwa Juni 3, mwaka huu pale Stade du 5 Juillet jijini Algiers nchini Algeria, Young Africans inapaswa kupata ushindi wa uwiano wa mabao 2-0 ili kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika, huku USM Alger ikihitaji sare ama ushindi kufanikisha azma ya kutawazwa kuwa mabingwa wapya wa Michuano hiyo.

Chivaviro apiga chini ofa ya Al-Akhdar
Simba SC, Young Africans zaiangusha Singida B.S