Watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU) katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wameanzisha mradi wa kufuga kuku na kilimo cha bustani ya mboga za majani ili kujikwamua kimaisha.
Mwenyekiti wa kikundi cha Jitambue kinachowaunganisha watu hao, Ester kilili, ameliambia majira kuwa wameamua kuunda kikundi hicho na kufuga kuku aina ya saso, baada ya kuona ni kitegauchumi ambacho kitawaingizia kipato na kuboresha afya zao hivyo kuacha kuwa tegemezi.
Amesema pia licha ya kuwapatia kipato pia kuku hao huwasaidia kuzalisha mbolea ambayo hutumika katika masuala ya kilimo kama bustani za mbogamboga wanazolima kwaajili ya chakula na kuboresha Afya zao wenyewe bila kutegemea wasaidizi.
Na ametoa wito kwa watu wanaoishi na VVU, wasikate tamaa ya maisha bali wajiunge na vikundi ili waweze kujikwamua kimaisha na kuondokana na dhana ya kuonekana wametengwa na jamii inayo wazunguka.
Naye Diwani wa kata hiyo, Zena Mijinga amesema kuwa nivigumu kwa watu waishio na VVU kujiunga na kutangaza kwamba wao ni wagonjwa, hivyo anakipongeza kikundi hicho kwa juhudi waliyonayo.
Na kusisitiza kuwa yupo pamoja na kikundi hicho kuwasaidia kupata baadhi ya misaada ambayo itaingia katika kata yake kwani wameonesha mfano mkubwa kwa jamii inayowazunguka kwa kuamua kujihusisha na ujasiriamali.