Mabingwa wa masumbwi wa dunia wa uzito wa juu, Deontay Wilder na Tyson Fury wataitikisa dunia ya masumbwi, watakapopanda ulingoni jijini Las Vegas nchini Marekani, leo (alfajiri ya kuamkia Kesho kwa saa za Afrika Mashariki).
Wababe hao ambao hawajawahi kupoteza pambano hata moja, watakata mzizi wa fitna na majigambo ya miaka miwili kati yao kujua nani atakuwa mbabe zaidi.
Fury amesafiri kutoka Uingereza na kumfuata Wilder nchini Marekani akiahidi kurudi na mkanda wa ubingwa wa dunia, lakini Wilder ameahidi kumzimisha na kwamba asiwaze kuzimaliza raundi 12.
“Naona muda hauendi, nasubiri kuona mwili wako unavyotetemeka juu ya sakafu ya ulingo baada ya kukuzimisha kwa ngumi yangu moja,” alisema Wilder katika tambo zake mbele ya Fury. “Baada ya kesho, kutakuwa na sura moja tu, na jina moja tu la bondia bora zaidi duniani wa uzito wa juu ambaye ni mimi, Deontay Wilder,” aliongeza.
Naye Tyson Fury amekuwa akimtambia Wilder akidai kuwa baada ya pambano hilo atamsaidia kuwa maarufu nchini Uingereza na Marekani kwa kumpiga vibaya ili atambulike kuwa alikutana na ngumi ya mbabe huyo.
“Mimi ndiye Mfalme na Mfalme ni mmoja tu. Mfalme ameingia Marekani, nitampiga Wilder na kumpa umaarufu kwa sababu najua hatambuliki. Nikimuangalia naona anaogopa sana, anaogopa nitakachomfanya hasa akikumbuka nilichomfanya Wladimir Klitschko.
Ingawa utabiri wa mshindi wa pambano hilo umekuwa mgumu kwa wengi, Bingwa wa dunia, Anthony Joshua amesema kuwa anaamini Muingereza mwenzake, Fury atashinda kutokana na namna alivyowahi kumpiga Klitschko mwaka 2015.
Mshindi wa pambano hilo anatarajiwa kupambana na Joshua mwakani.
Wilder ameshinda mapambano yake yote 40, na kati ya hayo mapambano 39 alishinda kwa KO. Kwa upande wa Fury, ameshinda mapambano yote 27, na kati ya hayo 19 ameshinda kwa KO.