Kutokana na ongezeko la vitendo vya ubakaji Zanzibar, wajumbe wa kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Ustawi wa Jamii na Kamati ya Wanawake na Watoto imeomba watuhumiwa wa makosa ya ubakaji kubadilishiwa adhabu ya jela miaka 30 kutokana na adhabu hiyo kutoendana na madhara yatokanayo na kitendo hiko.
Katika mkutano huo wa Wajumbe na asasi za kiraia za kutetea haki za wanawake na watoto wamesema umefika wakati sasa adhabu ya kesi ya ubakaji iwe ni kifungo cha maisha au adhabu ya kifo kwa wahusikawa wa matendo hayo.
Mwenyekiti wa kamati ya wanawake na watoto, Dk.Mwinyihaji Makame, amesema ”Adhabu ya kifungo cha miaka 30 haiendani na athari za tendo la ubakaji kwa muathirika kwani mtoto huathirika kisaikolojia, kiakili na kimwili”.
Ameongeza kwa kusema mahakama za Zanzibar hazitoi adhabu hiyo kesi nyingi za ubakaji zimekuwa zikitolewa hukumu ndogo ya chini ya miaka saba au mtuhumiwa kuachiwa huru.
Pia aliongezea kwa kusema rushwa imetawala katika kesi za ubakaji, pia jamii imekuwa na ugumu katika kutoa ushahidi wa kesi hizo.
Hivyo basi asasi hizo zilitoa mapendekezo kuwa sheria zifanyiwe marekebisho hasa katika kesi za jinai ili kesi za kikatili dhidi ya watoto kuwa miongoni mwa kesi ambazo hazina dhamana.