Adhabu ya kifungo cha miaka 30 au maisha jela inayotolewa kwa watu wanaokutwa na hatia ya kulawiti, kubaka na kuwapa mimba wanafunzi inaonekana kutokuwa suluhisho kwa matatizo hayo katika jamii, kwa mujibu wa Imamu Msaidizi wa Msikiti wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Hassan Katanga.
Akizungumza Julai 28, 2019 katika kusanyiko la watoto wanaoishi katika mazingira magumu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Sheikh Katanga alisema kuwa kuna sababu kwa viongozi wa dini kumfikishia wazo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kuandaa sheria itakayohusisha pendekezo hilo.
“Viongozi wa dini tunajaribu kufikiria, tuna mpango wa kumfikishia Mheshimiwa Rais wetu John Magufuli kwamba ni vizuri hili lipitishwe, mwenye kufanya tabia chafu na mbaya kwa watoto wetu, badala ya kuwafunga miaka 30 au maisha jela ni vizuri hawa watu wakahasiwa,” alisema Sheikh Katanga.
Aliongeza kuwa adhabu ya kifungo jela inawaumiza zaidi wananchi kwakuwa wafungwa hutumia kodi za wananchi kula chakula na matunzo mengine.
Katika hatua nyingine, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amewaonya wanaofanya vitendo vya ubakaji na kujihusisha kimapenzi na wanafunzi kuwa watakumbwa na mkono wa sheria.
Ameeleza kuwa sababu kuu ya kufanya vitendo hivyo ni imani za kishirikina zilizoshamiri.
Aidha, Kamanda Matei amewaomba wazazi kuhakikisha wanawapa malezi bora watoto wao pamoja na kuwalinda dhidi ya mambo mabaya yanayofanywa na wahalifu.